Home Biashara Viongozi wa kidini Waislamu na wa kisiasa wapinga Muguka

Viongozi wa kidini Waislamu na wa kisiasa wapinga Muguka

0

Viongozi wa dini ya Kiislamu na wale wa kisiasa ambao ni waumini wa dini hiyo, wamepaaza sauti kuhusu mjadala unaoendelea kuhusu zao la Muguka.

Kwenye taarifa baada ya mkutano wao katika ukumbi wa msikiti wa Jamia, viongozi hao waliitaka serikali kuu kuwa na ukweli inaposhughulikia suala hilo kwani zao la Muguka lina chembechembe zinazolifanya kuwa dawa ya kulevya kulingana na shirika la kupambana na matumizi ya pombe na mihadarati nchini, NACADA.

Viongozi hao walisema pia kwamba kulingana na ratiba ya nne ya katiba ya Kenya, masuala ya afya na biashara yamegatuliwa na hivyo serikali za kaunti za Mombasa, Kilifi, Taita Taveta, Lamu na Kwale zilichukua hatua sawa zilipopiga marufuku zao hilo.

Huku wakitambua tofauti za kitamaduni zilizopo kati ya watu wa jamii mbalimbali nchini, viongozi hao walisema kwamba nguvu za taifa zipo katika kukumbatia na kusherehekea tofauti hizo.

Hiyo walisema ndiyo sababu ambayo iliwachochea kutoa maoni yao kuhusu suala zima la zao la Muguka huku wakiitaka serikali kutumia nguvu sawa inaposhughulikia zao hilo ambalo athari zake zinafahamika jinsi inashughulikia matumizi ya pombe katika eneo la kati.

“Soko la Muguka linapoendelea kudidimia ulimwenguni, litakuwa jambo la busara kuunga mkono mabadiliko yanayolenga kuafikia mitindo bora na endelevu ya kilimo,” viongozi hao walisema katika taarifa hiyo ya pamoja.

Taarifa hiyo imetiwa saini na kamati ya msikiti wa Jamia, baraza kuu la Waislamu nchini, SUPKEM, shirika la Maahad Da’awah, mbunge wa Changamwe Omari Mwingi, mbunge wa kaunti ya Mombasa Zamzam Mohamed na Seneta wa Mombasa Faki Mohammed.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here