Home Kaunti Viongozi wa Baringo waazimia kushirikiana ili kukuza maendeleo

Viongozi wa Baringo waazimia kushirikiana ili kukuza maendeleo

Viongozi kutoka Kaunti ya Baringo wamedhamiria kuzika tofauti zao za kisiasa na kushirikiana wakati huu ambapo serikali inaendeleza kampeni za amani kwenye maeneo ambayo yamekuwa yakikumbwa na ghasia.

Wakizungumza katika shule ya msingi ya Kabartonjo iliyoko kaunti ndogo ya Baringo Kaskazini, viongozi hao walisema kuwa eneo hilo ambalo limekuwa likikumbwa na visa vingi vya wizi wa mifugo sasa linajivunia amani kutokana na juhudi za serikali na ushirikiano wa viongozi.

Seneta wa Baringo William Cheptumo alisema kuwa amani inadumishwa baada ya viongozi kusahau tofauti zao za kisiasa, kauli ambayo iliungwa mkono na Mbunge wa Tiaty, William Kamket.

“Umoja wetu ni muhimu sana Kwa sababu hapo awali viongozi hawakushirikiana katika majuku yao, lakini sasa tunafanya kazi kwa Umoja,” alisema Cheptumo.

Matamshi ya Cheptumo yaliungwa mkono na mbunge wa Tiaty William Kamket, alisema kuwa viongozi wote wa Baringo wameweka kando tofauti zao na kushirikiana kuanzia kwa Gavana hadi kwa viongozi wa mashinani, kwa maslahi ya maendeleo.

Viongozi hao walisema haya wakati wa ziara ya Rais William Ruto katika eneo hilo ambapo aliongoza shughuli ya utoaji hatimiliki 8,600 za mashamba na kuzindua ukarabati wa barabara ya kutoka Mogotio kuelekea Ziwa Bogoria-Kapkitur-Kisanana na Kamukunji.

Rais alidokeza kuwa wakati umewadia wa kutokomeza wizi wa mifugo katika eneo hilo.