Viongozi wa muungano wa Azimio-One Kenya wakiongozwa na Kalonzo Musyoka na Martha Karua, wamekashifu ukatili wa polisi dhidi ya wananchi ambao kulingana na viongozi hao walikuwa wakitekeleza haki yao ya kikatiba ya kuandamana.
“Katiba ya taifa hili inaelezea bayana kuhusu haki za kuandamana kwa amani. utumizi wa nguvu kupita kiasi haufai na ni kinyume na katiba,”alisema Kalonzo.
Viongozi hao walidokeza kuwa maandamano ya Azimio-OKA, ni ya amani na yanalindwa na katiba, huku wakisikitika kuwa maafisa wa polisi waliwadhulumu wananchi badala ya kuwalinda.
Viongozi hao walizungumza walipowatembelea waliojeruhiwa katika maandamano ya Jumatano waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya shalom na ile ya Machakos level 4.
Kulingana na Kalonzo, waathiriwa hao wanasema walikuwa katika shughuli zao za kawaida, kabla ya polisi kuwapiga risasi.
“Wengi walipigwa risasi kutoka nyuma, bila kujua kilichokuwa kikijiri,”alifoka Kalonzo.
Viongozi wengine pia waliwalaumu maafisa wa polisi, huku wakitangaza kurejelewa kwa maandamano Jumatano ijayo.