Vijana katika eneo la Nyahururu wameanzisha shughuli ya upanzi wa miche ya miti katika eneo chepechepe la manguo lililo karibu na mji wa Nyahururu.
Florence Koskei kiongozi wa vijana hao alisema kwamba mpango huo unawiana na wiki ya kimataifa ya vijana inayoendelea ambayo kauli mbiu yake inahimiza vijana kubuni mbinu za maendeleo endelevu kidijitali.
Koskei alisema kando na upanzi wa miche hiyo ya miti, wanapanga kunadhifisha mitaa ya mabanda ya Maina na Manguo iliyo karibu na mji wa Nyahururu.
Wanapoadhimisha wiki hiyo ya vijana wanapanga pia kuhamasisha wanarika wenzao kuhusu athari za matumizi mabaya ya pombe na dawa nyingine za kulevya.
Miche zaidi ya 300 tayari imepandwa na vijana hao katika eneo la Manguo nia ikiwa kuhifadhi mazingira katika eneo hilo ambalo ni makazi ya wanyama aina ya viboko.
Naibu chifu wa mtaa wa Manguo Chege Njoroge alisisitiza haja ya vijana kuungana hasa wakati huu ambapo utulivu umerejea baada ya maandamano ya Gen Z kuhimiza umoja na maendeleo.
Matamshi yake yaliungwa mkono na Collins Matasi na Simon Gathuo wawakilishi wa vijana wa mitaa ya Maina na Nanyuki mtawalia.