Home Kaunti Vijana Mandera watoa misaada kwa walemavu

Vijana Mandera watoa misaada kwa walemavu

0

Ulimwengu ulipokuwa ukiadhimisha siku ya walemavu jana Jumapili, kundi la vijana katika kaunti ya Mandera liliamua kujiunga na maadhimisho hayo kwa njia ya kipekee.

Kundi hilo kwa jina “Asal Generation Achievers Organization” liligawa vyakula kama mchele, sukari na mafuta ya kupikia kwa walemavu katika kaunti ya Mandera.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Mohammed Rashid, mmoja wa vijana hao alisisitiza haja ya usaidizi kwa walemavu katika jamii akiwataja kama watu ambao wako kwenye mazingira magumu.

Rashid aliomba makundi ya kijamii kama hilo lao na mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana kuchangia juhudi za kibinadamu kwa watu wasiobahatika katika jamii.

Mwenyekiti wa chama cha walemavu katika kaunti ya Mandera Ibrahim Ahmed, alishukuru vijana hao kwa msaada ambao alisema uliwasilishwa wakati mwafaka ambao ni siku yao ulimwenguni.

Aliomba serikali na wahisani wengine wote kuwasaidia kwa kuwapatia vifaa kama vile vya kuwasaidia kujitegemea.

Kulingana na takwimu, zaidi ya watu bilioni 1.3 ulimwenguni sawa na asilimia 16 ya idadi jumla ya watu ulimwenguni wana ulemavu na hivyo ni muhiumu kuwakumbuka kila mara na kutoa uhamasisho kwa jamii kuwahusu na kutetea haki zao.

Website | + posts