Home Kimataifa Vijana kaunti ya Mombasa wahamasishwa dhidi ya mihadarati

Vijana kaunti ya Mombasa wahamasishwa dhidi ya mihadarati

Mkutano huo uliwahamasisha vijana hao kuhusu jinsi ya kudumisha amani hapa nchini, ili kuwawezesha kufanikiwa katika nyanja zote maishani.

0
Vijana washiriki mkutano wa uhamasisho, kaunti ya Mombasa.
kra

Baraza la maimamu na wahubiri hapa nchini  (CIPK), limechukua hatua za haraka kuwahamasisha vijana dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.

Akizungumza katika ukumbi wa Tononoka wakati wa mkutano wa kuwahamasisha vijana, katibu wa baraza hilo  Sheikh Mohamad Khalifa, alisema lengo kuu la mkutano huo ni kuwaelimisha vijana jinsi ya kujikinga na matumizi ya mihadarati na madhara yake.

kra

“Pia tunawaonya dhidi ya kutumiwa na wanasiasa au yeyote yule kuzua ghasia, kuwatusi wanasiasa wengine, kuvuruga mikutano au kushiriki maandamano na uharibifu wa mali,” alisema Sheikh Khalifa.

Aidha mkutano huo uliwahamasisha vijana hao kuhusu jinsi ya kudumisha amani hapa nchini, ili kuwawezesha kufanikiwa katika nyanja zote maishani.

“Tunawataka wadumishe amani wakati wa likizo ya mwezi Agosti. Wale ambao huhudhuria madrassas, wafanye hivyo, na wale ambao huwa hawahudhurii wawasaidie wazazi wao kwa kazi za nyumbani,” aliongeza Sheikh Khalifa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kitaifa wa CIPK Abdalla Ateka, alisema baraza hilo linalenga kuanzisha mikutano hiyo ya kuwahasisha vijana katika kaunti zote 47.

“Tunawataka vijana kuwajibika. Hakuna taifa ambalo litastawi bila kuwa na vijana wanaowajibika, lakini iwapo tutakuwa wavivu na kujihusisha na matumizi ya mihadarati, taifa litaangamia,” alisema Ateka.

Mkutano huo uliwahusisha vijana kutoka Mvita, Kisauni, Likoni, Changamwe, Nyali na  Jomvu, ambao wana umri wa kati ya miaka 15-30.

Website | + posts