Idadi ya vifo kutokana na mkasa wa mlipuko wa gesi katika kijiji cha Mradi eneo la Embakasi, kaunti ya Nairobi imeongezeka hadi 6.
Hii ni baada ya watu watatu zaidi kufariki wakipokea matibabu kutokana na majeraha mabaya waliyopata kwenye mkasa huo.
Hatibu wa serikali Isaac Mwaura ametoa taarifa kuhusu mkasa huo akisema kuna wahasiriwa wengine 7 wa mkasa huo walio katika hali mahututi hospitalini.
Katika hospitali ya rufaa ya Kenyatta, majeruhi waliopelekwa huko ni 67 ambapo 6 kati yao walikuwa na majeraha mabaya ya kuchomeka. 27 wametibiwa na kuruhusiwa kuondoka huku 34 wakiendelea kupokea matibabu.
Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta imehudumia majeruhi 27 ambapo 8 wameruhusiwa kuondoka na 19 bado wanapokea matibabu.
Kulingana na Mwaura, serikali itaendelea kusaidia familia ambazo zilipoteza makazi yao kufuatia moto uliozuka baada ya gesi kulipuka.
Familia hizo sasa zimefikia 761 kutoka 663 zilizokuwa zimesajiliwa awali. Wengi kati ya watu hao wametafuta makazi mbadala huku familia 28 zikihifadhiwa katika ukumbi wa jamii huko Embakasi.
Waliopoteza stakabadhi muhimu kwenye mkasa huo wamehimizwa kujisajili katika ukumbi wa jamii wa Embakasi ili wapatiwe nakala zingine na mashirika husika.
Shirika la Msalaba Mwekundu limejitolea kulipia familia zilizoathirika kodi ya nyumba ya miezi miwili ambayo ni sawa na shilingi elfu 6.
Wamiliki wa nyumba hizo za kukodisha wanaombwa kuwavumilia wahasiriwa hao na wasiwatoze fedha zaidi ikitizamiwa hali yao ya sasa.