Home Kaunti Uwanja wa Dandora afueni kwa vijana wa Nairobi

Uwanja wa Dandora afueni kwa vijana wa Nairobi

Kwa miaka mingi ndoto ya kuwa na uwanja wa kisasa wa michezo katika eneo la Dandora ilikuwa kama mluzi wa mbali ambao unaathiriwa na upepo.

Lakini sasa furaha inadhihirika huku ujenzi wa uwanja huo ukikaribia kuisha, ishara ya mabadiliko katika maisha ya vijana na kandanda ya Nairobi.

Mlezi wa vijana Nairobi Steve Nzusa anasema kuna mwanga sasa na eneo la Dandora litabadili taswira kutoka kuwa chimbuko la wahalifu na kuwa chimbuko la wachezaji bora wa soka.

“Talanta zitakuzwa huku na sasa Dandora ina uwezo wa kubadilisha sifa zake kutoka kuwa eneo la uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya na kuwa eneo la ndoto za vijana wengi kutimia.” alisema Nzusa.

Maono kamili:

Uwanja wa michezo wa Dandora ulitizamiwa kuwa wa kisasa na una vifaa stahiki ambavyo vinaweza kumotisha kila mchezaji. Uwanja huo una nyasi bandia, viti vya ubora wa hali ya juu vitakavyokaliwa na maelfu ya mashabiki, taa za kumulika wakati wa michezo ya usiku na ukumbi wa kisasa wa mazoezi.

Huu sio wanja tu, ni eneo la kuzindua ndoto za wengi.

Mwanasoka Hillary Alaka anapongeza serikali kuu na ile ya kaunti ya Nairobi kwa mradi huu akisema ni hatua inayofaa katika kutambua talanta na kuzikuza ziwe za kiwango cha kimataifa.

“Ninapongeza serikali kwa kutekeleza mradi huu hata ingawa umechukua muda mrefu. Ombi langu ni kuwa miundomsingi iboreshwe kote nchini ili kusaidia kukuza talanta zaidi.” alisema Alaka

Zaidi ya matokeo:

Kando na mabao na makabiliano uwanjani, uwanja wa michezo wa Dandora unawakilisha fursa. Unatoa nafasi salama kwa wakazi wa umri mdogo wa Nairobi kukuza talanta zao, kujizoesha kushirikiana na wenzao, kuhimiza nidhamu na kuzoea mashindano mazuri.

Sasa timu za eneo la Dandora na maeneo ya karibu zimepata uwanja mzuri wa nyumbani ili kuandaa mashindano na kuwasha moto wa matumaini kwa wanaopania kuwa wanamichezo.

Athari za uwanja huu ni zaidi ya eneo la kuchezea, fursa za ajira, uimarishaji wa biashara zilizo karibu na nguvu mpya kwa jamii.

Trizah munyeki mkereketwa wa masuala ya soka anahisi kwamba uwanja wa michezo wa Dandora ni muhimu kwa vijana wanamichezo hasa wanajihusisha na soka.

“Uwanja huu utasaidia sio tu wapenzi wa michezo bali pia kuimarisha ari yao ya michezo kwani muundomsingi ni wa kuridhisha.” alisema Trizah

Bao la kusherehekewa:

Ukamilishaji wa uwanja huu uliosubiriwa kwa hamu ni ushindi kwa kila mmoja. Ni dhihirisho la ushirikiano kati ya serikali, viongozi wa jamii na wananchi waliokataa kuachilia ndoto hiyo ipotee.

Huku mluzi wa mwisho wa ujenzi wa uwanja huo ukikaribia kupigwa, huu sio mwisho tu wa Mradi, ni mwanzo wa sura mpya kwa michezo Nairobi.

Kuwa ange kwa ufunguzi rasmi kwa sababu utepe utakapokatwa kuashiria ufunguzi huo, utepe wa matumaini na ndoto za kizazi kizima nao utakuwa umekatwa.

Website | + posts
Hillary Murani
+ posts