Naibu Rais Rigathi Gachagua leo Ijumaa ametoa wito kwa mahafali kujitosa katika ujasiriamali hata wakati serikali ikiendelea kuweka mipango ya kubuni nafasi za ajira.
Gachagua pia ametoa wito kwa taasisi za elimu ya juu kuangazia kozi zinazokidhi mahitaji ya soko na zinazotosheleza mahitaji ya kiuchumi ya nchi kwa sababu kazi za ofisini zimekuwa zikipungua kila mwaka.
Aliyasema hayo wakati wa mahafali ya pamoja ya 40 ya Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia (JKUAT) na ya 9 ya Taasisi ya Teknolojia ya Sayansi na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha PanAfrican (PAUSTI) yaliyofanyika katika kaunti ya Kiambu.
Wanafunzi 4,299 walihitimu wakati wa hafla hiyo.
Naibu Rais alisema serikali inafanya mipango ya kubuni nafasi za ajira za kidijitali.
“Tunaweka miundombinu, taasisi za mafunzo zinapaswa kutoa ujuzi unaohitajika kwa vijana kuwa wafanyakazi wa dunia hata kutoka kwenye vijiji vyao. Teknolojia ipo hapa kuibadilisha ofisi ya dunia na kuiweka hadi kwenye viganja vyetu,” alisema Gachagua.
Huku akitoa wito kwa mahafali kujitosa katika biashara, Naibu Rais alisema kuna fursa nyingi za ujasiriamali.
Aidha aliwataka kuwa na shabaha maishani na kutumia ujuzi waliopata chuoni kuboresha maisha yao.