Home Habari Kuu Uteuzi wa Olimpiki katika riadha kuandaliwa uwanjani Nyayo

Uteuzi wa Olimpiki katika riadha kuandaliwa uwanjani Nyayo

0

Chama cha Riadha kimetangaza kuandaa majaribio ya kitaifa kuteua kikosi cha Kenya kwa makala ya 31 ya Olimpiki baina ya tarehe 14 na 15 mwezi huu, katika uwanja wa taifa wa Nyayo.

Kulingana na Afisa wa kamati kuu ya AK Barnaba Korir, wanariadha wote watapewa fursa sawa wakati wa majaribio hayo katika mashindano yaliyosalia, baada ya uteuzi wa mbio za mita 10,000 kuandaliwa Jumamosi iliyopita katika mashindano ya Prefontaine Classic Diamond League nchini Marekani .

“Leo tumekuwa na mazungumzo na wanariadha ili kubaini jinsi tunavyoweza kuwasaidia, ili waafikie matokeo bora katika michezo ya Olimpiki ya mwaka huu jijini Paris Ufaransa.Kesho tutakutana na wanariadha wa mbio za masafa marefu mjini Eldoret wanaojindaa kwa Olimpiki huku Kenya ikilenga kutetea matai yote mawili.”akasema Korir

Riadha Kenya pia imewahakikishia wanariadha kuwa majaribio ya kitaifa ya Olimpiki ya siku mbili, yataandaliwa katika uwanja wa Nyayo na sio ule wa Ulinzi Complex, ilivyotangazwa awali,baada ya Wizara ya michezo kukabali ombi la AK kutaka uteuzi huo uandaliwe katika uwanja huo ulioidhinishwa na shirikisho la Riadha Ulimwenguni.

“Wanariadha wanapaswa kumakinika kwa sasa baada ya kukubaliana na Wizara ya michezo ambayo imeturuhusu kutumia uwanja wa Nyayo kwa majaribo hayo ya siku mbili .Hali hii itatuwezesha kupata kikosi thabiti kwa Olimpiki.”akaongeza Korir

Bingwa mara mbili wa mbio za nyika Beatrice Chebet alivunja rekodi ya dunia ya mita 10,000 katika mashindano ya Prefontaine Classic wiki jana na kufuzu kwa Olimpiki kwa mara ya kwanza .

“Mashindano ya Prefontaine Classic yalikuwa ya kufana na tunaishukuru serikali ambayo ilituwezesha kutuma kikosi kikubwa cha mita 10,000 kamanjia ya kuhakikisha tunapata kikosi madhubuti,kitakachowezesha Kenya sio tu kushindana bali pia kunyakua dhahabu telezi.”akasisitiza Korir

AK pia imethibitisha kuwa wanariadha wawili bora katika mashindano ya prefontaine clasic wiki jana watafuzu kwa Olimpiki huku mwanariadha wa tatu akiteuiwa na jopo la maafisa wa kiufundi.

Kenya itawania kunyakua dhahabu ya kwanza ya Olimpiki ya wanawake katika mbio za mita 10,000 mwaka huu, na ya pili kwa wanaume tangu marehemu Naftali Temu atwae ubingwa mwaka 1968 nchini Mexico.

Mashindano ya Riadha kwenye Olimpiki ya mwaka huu yataandaliwa baina ya Agosti 1 na 11 mwaka huu jijini Paris Ufaransa.

Website | + posts