Home Habari Kuu Utafiti wa Infotrak: Gharama ya juu maisha mwiba kwa Wakenya wengi

Utafiti wa Infotrak: Gharama ya juu maisha mwiba kwa Wakenya wengi

0

Gharama ya juu ya maisha ni suala kuu linalowakwaza Wakenya wengi, kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni uliotolewa na kampuni ya Infotrak. 

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 93 ya Wakenya walilalamikia gharama ya juu ya maisha mwezi Disemba, 2023, idadi hiyo ikiongezeka kwa asilimia 4 ikilinganishwa na mwezi Septemba.

Asilimia 93 ya Wakenya pia walilamikia kupanda kwa gharama ya maisha katika utafiti uliofanywa mwezi Julai.

Hata hivyo, siyo gharama ya juu ya maisha pekee inayowafanya Wakenya wengi kukosa lepe la usingizi.

Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, asilimia 37 walilalamikia ukosefu wa ajira ikiwa ni ongezeko la asilimia 3 ikilinganishwa na mwezi Septemba huku asilimia 20 wakisema wameelewa na umaskini.

Utafiti huo wa Infotrak ulifanywa katika kaunti zote 47 kati ya Disemba 18 – 19 huku watu 1,500 wakihojiwa.

Utafiti huo ukija wakati ambapo serikali imewataka Wakenya kuwa na subira wakati ikitekeleza mikakati kabambe inayokusudia kukabiliana na hasa suala la gharama ya juu ya maisha.

Kinara wa Azimio Raila Odinga amekuwa mstari wa mbele kuisuta serikali kwa kufanya gharama ya juu ya maisha kupanda mno kutokana na kuongezwa kwa ushuru.

Raila ameashiria kuwa anawazia tena kuitisha maandamano mwaka 2024 ili kuishinikiza serikali kuangazia suala hilo.

Hata hivyo, Seneta wa Nandi Samson Cherargei amepuuzilia mbali kauli za Raila akimtaka kukoma kuwapotosha Wakenya kuhusiana na masuala ya uchumi.

Kwa mujibu wa Cherargei, uchumi wa nchi unaimarika taratibu na utakuwa bora hata zaidi mwakani.

Anaongeza kuwa hili linadhihirika wazi kutokana na uwezo wa Kenya kulipa madeni yake wakati nchi zingine zikishindwa.

Website | + posts