Home Biashara Infotrak: Asilimia 73 ya Wakenya wameathiriwa na hali ngumu ya kiuchumi

Infotrak: Asilimia 73 ya Wakenya wameathiriwa na hali ngumu ya kiuchumi

0

Utafiti wa hivi punde uliofaywa na kampuni ya Infotrak unaonyesha kuwa asilimia 73 ya Wakenya wanakabiliwa na hali ngumu kiuchumi. 

Kwa mujibu ya utafiti huo, asilimia 18 ya Wakenya waliohojiwa walisema wanakabiliwa na changamoto za kifedha, asilimia 55 walisema wanahangaika kukidhia mahitaji yao ilhali ni asilimia 5 tu waliosema hawakabiliwi na changamoto za kiuchumi.

Utafiti huo unaashiria kuwa hali ya kiuchumi sasa inaanza kuwa na athari kwa maisha ya Wakenya.

Kulingana na utafiti huo, asilimia 48 ya waliohojiwa walielezea kukumbwa na msongo wa mawazo na wasiwasi wakati asilimia 32 wakisema gharama ya juu ya maisha imekuwa na athari kwa uhusiano wao wa kibinafsi. Asilimia 21 walisema wamekuwa na matatizo ya kiafya ya kimwili wakati asilimia 18 wakishtakia kukumbwa na matatizo ya kiakili.

Na zikiwa zimepita siku 22 pekee tangu kuanza kwa mwaka mpya wa 2024, Wakenya wengi walielezea hofu kuwa hali ya maisha itaendelea kuwa ngumu zaidi kiasi kwamba asilimia 67 walihisi karo itaongezeka.

Asilimia 56 wanahisi ukosefu wa ajira utaongezeka wakati asilimia 51 wakitabiri kuwa gharama ya nishati itaongezeka.

Utafiti huo ulifanywa kati ya Disemba 18-19 mwaka jana ukiwahusisha watu wazima 1,500 kutoka kaunti zote 47 nchini.