Home Taifa Ushuru uliopendekezwa wa mkate waondolewa

Ushuru uliopendekezwa wa mkate waondolewa

0
kra

Mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu fedha Kimani Kuria ametangaza kuondolewa kwa ushuru uliopendekezwa wa mkate kwenye mswada wa fedha wa mwaka 2024.

Akihutubia wanahabari katika ikulu ya Nairobi baada ya mkutano wa wabunge wa mrengo tawala wa Kenya Kwanza, Kuria alisema kwamba wamesikia kilio cha wakenya na wakachukua hatua.

kra

Ushuru mwingine ambao umetolewa kwenye mswada wa fedha wa mwaka 2024 ni pamoja na ushuru wa asilimia 2.5 wa magari, ushuru wa usafirishaji wa sukari, ushuru wa mafuta ya kupikia, ushuru wa kubadilisha sarafu na wa huduma nyingine za kifedha.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya fedha bungeni alitangaza pia kwamba gharama ya kutuma pesa kupitia rununu pia haitaongezeka ilivyopendekezwa awali.

Kuria alifafanua kwamba ushuru wa kimazingira almaarufu Eco Levy utatozwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje zikiwa zimekamilika.

Bidhaa zinazotengenezewa humu nchini yakiwemo magari hazitatozwa ushuru huo katika kile alichokitaja kuwa hatua ya kuchochea ukuaji wa viwanda humu nchini.

Haya yanajiri wakati ambapo ripoti ya mswada wa fedha wa mwaka 2024 inatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili bungeni leo alasiri huku wabunge wakianza kujadili mswada huo.

Usalama umeimarishwa nje ya majengo ya bunge na katika sehemu mbali mbali za jiji la Nairobi wakati wakenya wanapanga maandamano nje ya bunge kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here