Home Habari Kuu Ushauri wa Khalwale kwa Rais Ruto

Ushauri wa Khalwale kwa Rais Ruto

0

Seneta wa kaunti ya Kakamega Bonny Khalwale amemshauri Rais William Ruto awafute kazi waziri wa biashara, waziri wa kawi na washauri wake katika masuala ya uchumi.

Khalwale aliyasema hayo huko Kakamega kutokana na ongezeko la hivi maajuzi la bei ya mafuta.

Kiongozi huyo anasema wakati umewadia wa Rais kuondoa maafisa hao kutoka kwa serikali yake kwa kutowajibika.

Analaumu waziri Moses Kuria, waziri Davis Chirchir, David Ndii, Mohammed Hassan na Nancy Laibuni kwa gharama ya maisha ambayo inazidi kupanda Kila siku.

Alisema yeye alichaguliwa na wananchi kuwawakilisha na mawaziri hao pamoja na washauri wa Rais katika masuala ya uchumi waliteuliwa kulinda wananchi dhidi ya matatizo ya kiuchumi.

Mafuta aina ya Super Petrol kwa Sasa yanauzwa shilingi 211.64 kwa Kila Lita, dizeli shilingi 201 kwa kila lita huku mafuta taa yakiuzwa shilingi 202.13 kwa kila lita jijini Nairobi.

Wakenya wamekuwa wakishutumu serikali kwa ongezeko la bei ya mafuta shutuma ambazo waziri Kuria alipuuza huku akishikilia kwamba bei ya mafuta itazidi kupanda kutokana na hali ilivyo ulimwenguni kote.

Waziri wa kawi Davis Chirchir alifika mbele ya kamati ya bunge kuhusu kawi Ijumaa ambapo alisema kama serikali hawana uwezo wa kudhibiti bei ya mafuta.

Alisema bei ya mafuta ghafi imekuwa ikiongezeka katika soko la ulimwengu na kusababisha bei ya mafuta nchini kuongezeka.

Waziri Kuria alisema kupitia mtandao kwamba bei ya mafuta itakuwa ikiongezeka kwa shilingi 10 kila mwezi hadi mwezi February mwakani.

Website | + posts