Home Burudani Usalama waimarishwa katika tamasha za Muziki na filamu kaunti ya Embu

Usalama waimarishwa katika tamasha za Muziki na filamu kaunti ya Embu

Kaulimbiu ya mwaka huu ya tamasha hizo ni "Kufungua fursa za mageuzi ya kijamii na kiuchumi kupitia Drama na Filamu"

0
Tamasha za Filamu zaandaliwa kaunti ya Embu.

Serikali imeimarisha usalama katika maeneo yote ambako tamasha za michezo ya kuigiza na filamu za mwaka huu zinaandaliwa.

Haya ni kwa mujibu wa katibu mkuu wa tamasha za michezo ya kuigiza na muziki humu nchini James Indimuli.

“Hatujakuwa na visa vyovyote vya utovu wa usalama, lakini wizara ya usalama wa taifa, imewapeleka maafisa wa usalama katika maeneo yote ya tamasha hiyo,” alisema Indimuli.

Kulingana na Indimuli  wanafunzi 15,000 kutoka shule za msingi hadi vyuo vikuu, watashiriki katika tamasha hizo za mwaka huu.

Aidha, amesema wizara ya usalama wa taifa imepeleka maafisa wa usalama wa kutosha kuimarisha usalama katika makazi pamoja na maeneo ambako tamasha hizo zitaandaliwa.

Akizungumza Jumanne katika chuo kikuu cha Embu Kaunti ya Embu, ambako tamasha hizo zinaandaliwa, Indimuli alisema tamasha hizo zilizoanza Jumatatu wiki hii zitakamilika kwa tamasha ya kitaifa itayoandaliwa Alhamisi, wiki ijayo.

Aidha, Indimuli alisisitiza kuwa baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa kielimu unaozingatia mfumo wa umilisi, tamasha hizo sasa zina mchango mkubwa sana katika kuendeleza taaluma ya wanafunzi.

Kaulimbiu ya mwaka huu ya tamasha hizo ni “Kufungua fursa za mageuzi ya kijamii na kiuchumi kupitia Drama na Filamu”.

Website | + posts