Home Habari Kuu Usalama waimarishwa Azimio ikipanga kufanya maandamano

Usalama waimarishwa Azimio ikipanga kufanya maandamano

0

Usalama umeimarishwa kote nchini huku muungano wa Azimio ukipanga kufanya maandamano leo Ijumaa.

Muungano huo umeitisha maandamano hayo kushinikiza kubatilishwa kwa sheria ya fedha ya mwaka 2023.

Unadai isipobatilishwa, sheria hiyo iliyoanza kutekelezwa Julai 1, 2023, itafanya gharama ya maisha kuwaelemea Wakenya wengi.

Hata hivyo, mahakama kuu imetoa maagizo ya kusitisha utekelezwaji wa sheria hiyo hadi kesi iliyowasilishwa na Seneta wa Busia Okiya Omtatah isikilizwe.

Mapema leo Ijumaa, maafisa wa polisi waliwatawanya vijana kadhaa waliosomekana kutoka mtaa wa Mathare waliokuwa wameziba barabara ya Thika na kufanya isipitike.

Walikuwa wameyawasha moto magurudumu na pia walisemekana kuyarushia magari mawe.

Ni hali iliyokashifiwa vikali na Seneta wa kaunti ya Nandi Samson Cherargei.

“Vitendo vya uvunjaji wa sheria vilivyoripotiwa kwenye barabara ya Thika ni sawa na kuhujumu uchumi…Ikiwezekana, polisi wanapaswa kufuta maandamano na kukabiliana vikali na wanaovunja sheria na kuwakamata waliyoyapanga!” alisema Cherargei.

Wafuasi kadhaa wa Azimio tayari wanaelekea katika uwanja wa Kamukunji ambapo viongozi wa muungano huo wakiongozwa na Raila Odinga watafanya mkutano mkubwa.

Mjini Kisumu, wafanyabiashara wengi wamefunga biashara zao kwa hofu ya mali yao kuporwa.

Usalama pia umeimarishwa mjini Mombasa ambapo waandamanaji na wanaharakati kadhaa wanashiriki maandamano ya Saba Saba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here