Usajili wa makurutu wa jeshi la Kenya, KDF unaanza leo Jumatatu.
Utafikia kikomo Septemba 8, 2023 na utajumuisha usajili wa makurutu wa kawaida, walio na ujuzi katika nyanja mbalimbali, watakaopata ujuzi maalum, makurutu wa majukumu ya kawaida pamoja na makonstebo.
Kila anayetaka kusajiliwa kwenye jeshi lazima awe na kitambulisho cha kitaifa, asiwe na rekodi ya uhalifu, urefu wa mita 1.6 kwa wanaume na mita 1.52 kwa wanawake na uzani wa kilo 54 kwa wanaume na kilo 50 kwa wanawake.
Watahitajika kuwa wa umri wa kati ya miaka 18 na 26 kwa makadeti na makurutu wa majukumu ya kawaida.
Wanaolenga kusajiliwa kama wajuzi wa nyanja fulani hitajika na watakaopokea mafunzo ya nyanja fulani wasizidi umri wa miaka 30 na wawe na tajriba ya miaka angalau miwili katika nyanja zao.
Afya nzuri na ngozi yenye afya isiyo na makovu na michoro ni muhimu pia.
Wakenya wametahadharishwa pia wasijaribu kutumia mbinu haramu ili kushawishi usajili.