Home Habari Kuu Upepo mkali wavuma Kilifi

Upepo mkali wavuma Kilifi

0

Upepo mkali sana umeripotiwa katika maeneo mbalimbali ya pwani ya Kenya kutokana na dhoruba ya Tropiki IALY.

Kulingana Na shirika la msalaba mwekundu, upepo huo uliathiri eneo la Majajani kaunti ya Kilifi ambapo uling’oa paa la nyumba ya moja makazi.

Nguzo za umeme huko Casuarina, Olimpia, Madunguni huko Malindi na Garashi huko Magarini, Kaunti ya Kilifi, zilianguka huku nguzo mbili za Kituo cha biashara cha Jilore zikiwaka moto.

Hakuna majeruhi walioripotiwa kufikia sasa.

Shirika hilo la msalaba mwekundu linahimiza wakazi wa maeneo hayo kutahadhari kwani upepo huo huenda ukaathiri shughuli za baharini kwa kiwango kikubwa.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini Kenya ilikuwa imetoa tahadhari sawia ilipotoa utabiri wa Jumanne na Jumatano katika eneo zima la Pwani kufuatia dhoruba IALY.

Wavuvi walishauriwa kutokwenda kutekeleza shughuli zao katika maji makuu kwani huenda kukawa na athari.

Jemie Saburi
+ posts