Shule ya Upendo Friends iliyoko viungani mwa mji wa Arusha nchini Tanzania ni shule inayotoa mafunzo kwa wanafunzi wa viwango vya chekechea hadi shule ya msingi kwa wanafunzi wa kutwa na wale wanaoishi shuleni.
Tangu kuasisiwa kwake mnamo mwaka 2006 na Bi. Isabbella Mwampamba, shule hiyp imekuwa katika mstari wa mbele kutoa mafunzo ya kisasa na ya hali ya juu kwa maelfu ya wanafunzi.
Sio mafunzo tu bali pia shule ya Upendo Friends inamiliki Upendo Friends Sports Academy, iliyo maarufu kwa kukuza na kulea vipaji katika mkoa wote wa Arusha na mpakani mwa Kenya.
Katika akademia hii, wanafunzi hupokea mafunzo katika fani kadhaa za michezo ikiwemo kandanda na riadha kwa kiwango kikubwa, mafunzo yanayoendeshwa na wakufunzi waliohitimu.
Kando na wakufunzi, pia wanamichezo hususan wanariadha wastaafu kama Suleiman Mjao uhusishwa katika kuwamotisha wanamichezo chipukizi.
Ni kupitia kwa njia hii ambapo mashindano mawili maarufu yamekuwa mwanzo, yakiwa yale ya East Africa Sports Tourism Challenge ambayo yalianzishwa mwaka 2022 mkoani Geita.
Mashindano haya ambayo makala ya pili yataandaliwa mwezi Disemba mwaka huu, huwashirikisha chipukizi wa kutoka mataiafa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao hushindana, kutangamana na pia kukuza utalii.
Mwezi Juni mwaka huu, mashindano makubwa zaidi ya riadha kwa watoto yalizinduliwa mkoani Arusha, mashindano ya Watoto Festival yakiandaliwa na Bi Mwampamba.
Kando na kuwashirikisha takriban watoto 2,000 kutoka shule mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Arusha, pia mashindano hayo yaliwavutia watu wazima waliokuwa na ari kutazama watoto wakishindana katika fani mbalimbali.
Hata wadau pia waliyapa shavu mashindano hayo ya Juni ambayo kulingana na Bi. Mwampamba, wanalenga kuyaandaa kila mwaka na kuyapanua ili kuwashirikisha watoto kutoka shule za Afrika Mashariki.