Shughuli ya upasuaji wa maiti 21 za wanafunzi waliofariki kwenye mkasa wa moto katika shule ya Endarasha Hillside Academy, unatarajiwa kufanyika leo.
Hii inafuatia kukamilika kwa uchunguzi wa sampuli za wazazi za vinasaba, yaani DNA.
Upasuaji huo utasaidia kubaini chanzo cha vifo vya wanafunzi hao Ijumaa iliyopita, na pia kutambulisha miili kwa kulinganisha na sampuli za DNA zilizokusanywa kutoka kwa wazazi.
Uchunguzi ungali ukiendelea kubaini chanzo cha moto huo huku watu kadhaa wakirekodi taarifa kwa polisi wakiwemo mume na mke wanaomiliki shule hiyo.
Wanafunzi 19 waliaga dunia katika moto huo huku wengine wawili wakifariki hospitalini walipokuwa wakipokea matibabu.
Serikali pia imeamrisha kufanywa ukaguzi kwa shule zote za mabweni nchini, ili kuhakikisha zinaafiki viwango vya usalama vilivyowekwa.