Wakili Joe Khalende alijeruhiwa leo Jumatano, siku moja baada ya kujitangaza kuwa Katibu Mkuu wa chama cha UDA.
Hii ni baada ya wafuasi wake kuripotiwa kukabiliana na wale wa kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho Cleophas Malala.
Mwenyekiti wa UDA Cecily Mbarire amepuuzilia mbali hatua ya Khalende kujitangaza kumrithi Malala akisema chama hicho kina katiba na taratibu za kufuatwa katika kufanya mabadiliko yoyote ya uongozi chamani.
Akiwahutubia wanahabari jana Jumanne, Khalende alitangaza kufurushwa kwa Malala akimtuhumu kwa kuwa kibaraka wa maadui wa UDA.
Alimnyoshea Malala kidole cha lawama akidai amejiunga na vuguvugu la Tawe linaloendeshwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na ambalo amedai limekuwa likiipinga serikali.
Malala amepuuzilia mbali madai hayo.
“Puuza propaganda. Chama kiko imara na kimedhamiria kumsaidia Rais William Ruto kufikia ajenda yake kwa niaba ya nchi hii,” alisema Malala.
Awali, baadhi ya viongozi wa UDA akiwemo Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga waliapa kuwa watamfurusha Malala kutoka kwenye wadhifa huo.