Umoja wa Afrika, AU umetoa wito kwa washikadau wote humu nchini kuwa watulivu na kuepukana na vurugu.
Kupitia taarifa, mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC Moussa Faki Mahamat pia ametoa wito kwa washikadau wa kitaifa kushiriki mazungumzo yenye tija kwa lengo la kusuluhisha masuala tata yaliyosababisha maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.
Amesema hii inapaswa kufanyika kwa manufaa ya taifa hili.
“Mwenyekiti anasisitiza kusimama kikamilifu kwa Umoja wa Afrika na serikali na Wakenya na kutoa wito kwao kudumisha amani, usalama na uthabiti nchini humo,” alisema Mahamat katika taarifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia ametoa matamshi sawia akielezea kusikitika kwake kutokana na maafa yaliyoshuhudiwa nchini wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 jana Jumanne.
“Nimehuzunishwa mno na ripoti za vifo na majeruhi – wakiwemo wanahabari na matabibu – zinazohusiana na maandamano nchini Kenya,” alisema Guterres katika mtandao wake wa X.
“Natoa wito kwa mamlaka za Kenya kujizuia, na kutoa wito kwa maandamano yote kufanyika kwa njia ya amani.”