Home Habari Kuu Ulanguzi wa pesa watajwa kuwa ufadhili mkuu wa ugaidi

Ulanguzi wa pesa watajwa kuwa ufadhili mkuu wa ugaidi

Katika mkutano huo, ukaguzi wa utekelezaji wa mikakati kuhusu vita dhidi ya ugaidi ulifanyika.

0

Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki amesema Kenya inaendelea kuweka mikakati ya kukabiliana na tishio la ugaidi linaloweza kutekelezwa kupitia mitandao ya adui katika kanda hii na kimataifa.

Kindiki ambaye aliongoza mkutano kuhusu kupambana na ulanguzi wa fedha na kukabiliana na ufadhili wa ugaidi siku ya Jumatatu, alisema serikali imebaini ulanguzi wa fedha kuwa mojawapo ya njia maarufu zaidi za ufadhili wa ugaidi.

Katika mkutano huo, ukaguzi wa utekelezaji wa mikakati kuhusu vita dhidi ya ugaidi ulifanyika.

Mkutano huo ulioandaliwa katika afisi ya Waziri Kindiki jijini Nairobi, pia ulijadili mikakati mipya ya kutambua na kuzuia mtiririko wa fedha haramu.

Aidha uliazimia kukandamiza vyanzo vyote vya pesa za ulanguzi kama sehemu ya juhudi za kimataifa za kukabiliana na vitisho vya ugaidi vilivyopo na vinavyoibuka.

Miongoni mwa wale waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Gavana wa Benki Kuu Dkt. Kamau Thugge, Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome na Mkurugenzi Mkuu wa Uhamiaji Evelyn Cheluget.

Website | + posts