Home Habari Kuu Uhuru wa mahakama hauwezi ukaingiliwa kivyoyote, asema Jaji Koome

Uhuru wa mahakama hauwezi ukaingiliwa kivyoyote, asema Jaji Koome

0

Jaji Mkuu Martha Koome amepuuzilia mbali madai kuwa mazungumzo kati ya idara ya mahakama na mihimili mingine ya serikali yanaweza yakaathiri uhuru wa idara hiyo. 

Siku chache zilizopita, Jaji Koome alikuwa kiini cha shutuma baada ya kushiriki mazungumzo na Rais William Ruto na spika wa bunge la taifa Moses Wetang’ula katika Ikulu ya Nairobi.

Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana ambaye pia ni Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru ni miongoni mwa walioshiriki mkutano huo.

Upinzani na chama cha wanasheria nchini, LSK ni miongoni mwa waliolaani mkutano huo kwa hofu kuwa utakuwa mwiba kwa uhuru wa mahakama.

Hofu ambazo Jaji Koome amezipuuzilia mbali, akisema mazungumzo na mihimili mingine ya serikali kutatua changamoto kwa kusudi la kuhakikisha haki inatendeka hayawezi yakaathiri uhuru wa mahakama.

“Tunaweza tukashiriki mazungumzo yenye tija yanayowezesha taasisi kutekeleza wajibu wake ipasavyo, huku tukihakikisha hatushiriki mazungumzo yanayotuelekeza namna kesi mahakamani zinapaswa kuamuliwa,” alisisitiza Jaji Koome.

Jaji Koome aliyasema hayo leo Jumatatu wakati wa kuanza kwa mkutano wa siku tatu wa wakuu wa idara ya mahakama.

Uhuru wa mahakama, uboreshaji wa huduma na uongezaji wa uwajibikaji ni miongoni masuala yaliyotawala vinywa vya wengi wakati wa kuanza kwa mkutano huo utakaomalizika keshokutwa Jumatano.