Home Taifa Uhuru: Elimu ni muhimu kwa ustawi wa Afrika

Uhuru: Elimu ni muhimu kwa ustawi wa Afrika

0
Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta
Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta
kra

Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta amesisitiza umuhimu wa elimu katika kuhakikisha bara la Afrika linapiga hatua kimaendeleo. 

Amelitaka bara hilo kufanya uwekezaji mkubwa katika elimu na ukuzaji uwezo kwa ajili ya ustawi wake siku zijazo.

kra

“Elimu ndio tegemeo kuu kwa ajili ya watoto wetu kujikimu katika ulimwengu ambao daima unabadilika,” alisema Uhuru jana Alhamisi wakati wa Majadiliano ya Demokrasia ya Wakfu wa Goodluck Jonathan 2024 mjini Benin katika jimbo la Edo nchini Nigeria.

Maudhui ya majadiliano hayo mwaka huu yalikuwa; “Elimu Inayofaa na Uongozi Unaostahili wa Kisiasa kama Suluhisho la Ukuaji na Maendeleo ya Afrika.

Ni majadiliano yaliyowaleta pamoja viongozi wakuu wa kisiasa, watunga sera na wataalam kutoka barani Afrika kuangazia jukumu muhimu linalotekelezwa na elimu na kuchaguliwa kwa viongozi wanaofaa katika kufikia malengo ya maendeleo ya mataifa ya Afrika.

Wakati wa utawala wake, Uhuru alitoa kipaumbele kwa wanafunzi wote wa shule ya msingi kujiunga na shule za upili kwa asilimia 100, na hivyo kuhakikisha kila mwanafunzi alinufaika na fursa za masomo bila kujali uwezo wao wa kiuchumi na kijamii.

“Maono yetu na malengo yalikuwa kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi nchini Kenya amepata fursa sawa,” aliongeza Uhuru.

Wakfu wa Goodluck Jonathan uliasisiwa na Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan mnamo mwaka 2015 kwa lengo la kuhamasisha demokrasia, amani na mabadiliko barani Afrika.

Goodluck aliunga mkono matamashi ya Uhuru akisema elimu ndio msingi wa maendeleo ya taifa lolote lile.

“Bila msingi wa elimu thabiti, hatuwezi tukatarajia ukuaji endelevu,” alisema Jonathan.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here