Home Habari Kuu Uhuru awasili Afrika Kusini kuongoza waangalizi wa AU kabla ya Uchaguzi Mkuu

Uhuru awasili Afrika Kusini kuongoza waangalizi wa AU kabla ya Uchaguzi Mkuu

Uhuru atawaongoza wajumbe 60 wa Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AUEOM), katika shughuli za kuandaa uchaguzi huo.

0
Uhuru Kenyatta kuongoza waangalizi wa uchaguzi wa AU Afrika kusini.

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, amewasili Afrika Kusini kuongoza shughuli za uangalizi wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mnamo Mei 29, 2024.

Uhuru atawaongoza wajumbe 60 wa Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AUEOM), katika shughuli za kuandaa uchaguzi huo.

“Ujumbe huo utaingiliana na mamlaka za serikali, Tume Huru ya Uchaguzi, vyama vya siasa, vyombo vya habari, mashirika ya kiraia na wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa katika uchaguzi ujao wa 2024,” ilisema Umoja wa Afrika (AU) kupitia ujumbe.

Wajumbe hao walichaguliwa na AU baada ya serikali ya Afrika Kusini na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo (IEC) kuomba AU kusaidia katika uangalizi wa uchaguzi.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, aliidhinisha kutumwa kwa AUEOM ya muda mfupi ili kutathmini na kutoa ripoti kuhusu uendeshaji wa uchaguzi huo.

Waangalizi hao sitini wa AUEOM walichaguliwa kutoka kwa mabalozi walioidhinishwa kwa Umoja wa Afrika, maafisa wa mashirika ya usimamizi wa uchaguzi na wanachama wa mashirika ya kiraia ya Afrika.

Pia inajumuisha wataalam wa uchaguzi wa Afrika, wataalamu wa haki za binadamu, wataalam wa jinsia na vyombo vya habari na wawakilishi wa mashirika ya vijana.

Waangalizi hao wanatoka mataifa 24 ambazo ni pamoja na Angola, Benin, Botswana, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Misri, Ethiopia, Eswatini, Gambia, Ghana, Kenya, Lesotho, Mauritius, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Sudan Kusini, Togo, Tunisia, Uganda, Zambia na Zimbabwe.

Alphas Lagat
+ posts