Serikali haitalegeza kamwe sera yake ya kuwahamisha maafisa wa polisi 42, 000 waliohudumu katika kituo kimoja cha polisi kwa zaidi miaka mitatu.
Hadi kufikia sasa, maafisa 26,000 tayari wamehamishiwa vituo vipya.
Mchakato wa kuwahamisha maafisa 16,000 waliosalia unaendelea kwa sasa.
Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki aliyasema hayo leo Alhamisi alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Taifa juu ya Utawala na Usalama wa Ndani ili kujibu maswali mbalimbali kuhusiana na usalama humu nchini.
Hatua ya kuwahamisha polisi hao ilitokana na vilio vya raia vya mara kwa mara kuwa maafisa waliohudumu katika vituo mbalimbali kwa zaidi ya miaka mitatu wamezembea kazini.
Baadhi walinyoshewa kidole vya lawama kwa kula njama na magenge ya wahalifu na kuchangia ukosefu wa usalama katika maeneo yao ya utenda kazi.
Wakati huohuo, Waziri amedokeza kuwa serikali inatekeleza hatua mbalimbali zenye lengo la kukabiliana na mauaji ya wababodaboda na wizi wa pikipiki zao.
Hatua hizo zinajumuisha uongezaji wa ushikaji doria kote nchini ili kuzuia na kuwakamata wahalifu, kuhamasisha ulinzi wa jamii na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali za kaunti, maafisa wa utawala wa serikali kuu na usimamizi wa wanabodaboda nchini.