Ugonjwa wa kifua kikuu, yaani TB bado ni changamoto kubwa inayoibua mashaka kwa afya ya umma sio tu humu nchini bali kote duniani.
Katibu katika Wizara ya Afya amesema ugonjwa huo bado ni chanzo kikuu cha vifo vya watu wengi.
“Athari za ugonjwa huo kwa jamii na uchumi hazihesabiki, huku kuchipuka kwa ugonjwa sugu wa TB kukiongeza zaidi tatizo hilo,” alisema Katibu Muthoni wakati akizindua mpango wa mkakati wa TB wa mwaka 2023/24 – 2027/28 leo Jumatatu.
Hususan, Muthoni alilalamikia visa vinavyoongezeka vya ugonjwa huo humu nchini, huku vingine vikiwa bado havijatambulika.
Mathalan, mnamo mwaka 2022, visa 90, 841 vya TB viliripotiwa ikilinganishwa na visa 77,854 vilivyoripotiwa mnamo mwaka wa 2021.
“Ingawa idadi hii ni ya kutisha, inawakilisha tu asilimia 68 ya visa 133,000 vinavyokadiriwa vya TB vilivyotabiriwa kutokea mwaka huo, na kuacha asilimia 32 ya visa vikiwa havijatambuliwa na kutibiwa,” aliongeza Muthoni.
Aliuelezea mpango wa mkakati wa TB wa mwaka 2023/24 – 2027/28 kuwa ishara ya kujitolea kwa Wizara ya Afya kwa ushirikiano na wadau kusitisha athari za ugonjwa huo katika jamii.