Sasa imebainika kwamba ugonjwa ambao ulisababisha vifo vya takribani watu 17 nchini Uganda ni kimeta, kulingana na maafisa wa afya nchini humo.
Ugonjwa huo uliozuka katika wilaya ya Kyotera ulisababisha waathiriwa kupata vipele, kufura viungo na baadaye kuaga dunia.
Kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika awali kilikuwa kimetangaza kwamba ugonjwa huo hauwezi kuwa kimeta lakini vipimo vya waathiriwa nchini Uganda vimebainisha kwamba wanaugua kimeta.
Ugonjwa wa kimeta unaosababishwa na bakteria huathiri mifugo mara nyingi wakiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo lakini pia unaweza kuambukizwa binadamu.
Kufikia sasa, waathiriwa wapatao 40 wamebainishwa kuugua ugonjwa huo nchini Uganda.
Msimamizi wa masuala ya afya katika wilaya ya Kyotera Edward Muwanga alisema ni afueni kidogo kwa sababu sasa wamefahamu ugonjwa wanaokabiliana nao.