Magavana wanadai hawajapokea mgao wao wa fedha kutoka kwa serikali kuu kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita ukiwemo mwezi huu, ilhali kasi ya mfumo wa IFMIS huripotiwa kupungua katikati ya mwezi Juni.
“Ikiwa serikali kuu itazngatia sheria na kutupa rasilimali zetu tarehe 15 ya kila mwezi, hakuna kaunti itakuwa na deni la KEMSA,” alisema Njuki wakati akiwahutubia wanahabari.
“Deni si kitu kibaya. Isitoshe, makubaliano tulio nayo na KEMSA yanazipatia kaunti muda wa siku 90 kufanya malipo. Si muda huo unawiana na muda ambao kaunti hazijapokea mgao wa fedha zake?”
Baadhi ya watu wamependekeza serikali kuu kuchukua tena usimamizi wa sekta ya afya wakiwatuhumu Magavana kwa usimamizi mbaya wa sekta hiyo. Hata hivyo, Magavana wameapa kwamba kamwe hawataruhusu sekta hiyo iliyogatuliwa baada ya kupitishwa kwa katiba mpya ya mwaka 2010 kusimamiwa tena na serikali kuu wakitaja manufaa chungu nzima wanayosema yamepatikana kupitia ugatuzi.
KEMSA inasema inazidai kaunti kitita cha shilingi zipatazo bilioni tatu.