Home Habari Kuu Ufunguzi wa shule zilizoathiriwa na mafuriko kucheleweshwa

Ufunguzi wa shule zilizoathiriwa na mafuriko kucheleweshwa

0

Wizara ya usalama wa taifa imetangaza kwamba ufunguzi wa shule ambazo zimeathiriwa zaidi na mafuriko ambayo yamesababisha wengi kupoteza makazi katika sehemu mbali mbali za nchi, utacheleweshwa.

Katika taarifa, wizara hiyo ilisema kwamba makundi ya wawakilishi wa mashirika mbali mbali ya kitaifa na ya kaunti yatahakikisha kwamba ukarabati unafanywa ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi watakaporejelea masomo katika shule hizo.

Usalama pia umeimarishwa katika vituo vyote vya magari ya uchukuzi wa umma wanafunzi wanaporejea shuleni leo kwa muhula wa pili, ufunguzi ulioahirishwa kutokana na mafuriko.

Maafisa wa polisi wamewekwa katika vituo hivyo na maeneo mengine kuhakikisha usafiri unaendelea ipasavyo hasa wa wanafunzi wanaorejea shuleni.

Maafisa wa trafiki wamewekwa pia katika barabara zote kuu nchini ambapo watahakikisha sheria za trafiki zinafuatwa kama vile kasi inayostahili, idadi inayostahili ya abiria katika kila gari na kuondoa magari mabovu barabarani.

Magari hayatakubaliwa kutumia madaraja ambayo yametambuliwa kutokuwa salama pamoja na barabara zenye hatari.

Mito, mabwawa na maeneo mengine ya maji mengi yatakuwa chini ya uangalizi ili kutambua iwapo ni hatari kwa jamii zinazoishi karibu na miondomsingi muhimu.

Wazazi wa wanafunzi wa shule za kutwa wamehimizwa kuwajibikia usalama wa wanao wanapokwenda shule asubuhi na kurejea jioni, jukumu litakalotekelezwa ka ushirikiano na kamati za kimaeneo za usalama.

Awali ufunguzi wa shule ulikuwa umepangiwa Aprili 29, 2024 lakini ukaahirishwa mara mbili kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa.

Website | + posts