Home Michezo Ufadhili wa Shabana Fc waongezeka kufuatia ushindi

Ufadhili wa Shabana Fc waongezeka kufuatia ushindi

0
Timu ya Shabana yashinda timu ya NSL. Picha/Hisani

Mfadhili wa timu ya soka ya Shabana Fc ya Kisii ameahidi kuongeza ufadhili huo kutoka milioni 20 za awali kufuatia ushindi wa timu hiyo. Timu hiyo ilinyakua ubingwa wa ligi ya NSL, msimu wa mwaka 2022/2023 Jumamosi Julai 8, 2023 baada ya kuishinda timu ya Kisumu All stars mabao 2 kwa 0 katika uwanja wa Gusii.

Huku akipongeza timu hiyo, Gavana Simba Arati ambaye amekuwa kwenye ziara nchini China ameelezea kupitia ukurasa wake wa Facebook kwamba mfadhili wa Shabana ambaye alimtafuta mwenyewe ameahidi kuongeza ufadhili na kwamba atasafiri hivi karibuni kutoka China hadi Kenya ili kuweka mikakati zaidi ya kusaidia timu hiyo.

Timu ya Shabana sasa imepandishwa ngazi kutoka ligi ya NSL hadi ligi ya FKF- KPL, msimu ujao na Gavana Simba anaitakia kila la heri.

Kiongozi huyo wa gatuzi la Kisii alielezea kwamba alisaidia timu ya Shabana kupata uwanja wa michezo wa Gusii kwa matumizi kama wanja wao wa nyumbani bila malipo na akaikubalia kukusanya mapato kutoka kwa mashabiki langoni kama kiingilio ili kujikimu. Anafurahia kwamba hatua aliyochukua imezaa matunda.

Gavana Simba anasema uwanja wa Gusii utaendelea kukarabatiwa na kufanywa bora ili uendelee kutumika kwa ajili ya michuano ya soka na kwa ajili ya michezo mingine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here