Rais William Ruto amesisitiza kuwa serikali yake itatekeleza mpango wa nyumba za bei nafuu.
Amesifia mpango huo akisema tayari umetekelezwa katika mataifa mengine ambayo yamepiga hatua kubwa kimaendeleo.
“Tutakeleza mpango wa nyumba za bei nafuu. Sitaki kusema ni kwa njia yoyote ile inayowezekana, nimesema tu tutautekeleza, kwa sababu hicho ndicho kitu ambacho mataifa mengine yaliyoendelea yamefanya,” alisema Rais Ruto katika hotuba yake wakati wa mkutano wa siku nne wa viongozi wa serikali kuu wakiwemo mawaziri na wabunge wa Kenya Kwanza unaofanyika mjini Naivasha.
“Hata kwa wale wanaopinga mpango wa nyumba za bei nafuu, siyo kwa sababu kwamba hawajui hicho ndicho kitu sahihi cha kufanya. Shida yao ni kwamba ni sisi tunaoutekeleza wala sio wao.”
Mpango wa nyumba za bei nafuu umekumbana na visiki vya kisheria katika idara ya mahakama huku mahakama ya rufaa ikiagiza kusitishwa kwa utozaji wa kodi ya nyumba hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani inayopinga wafanyakazi kutozwa ada hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Katika uamuzi wake, jopo la majaji watatu wa mahakama kuu liliitaja kodi hiyo kuwa kinyume cha sheria na kukosoa mpango huo kwa kukosa sheria stahiki ya kuongoza utekelezaji wake.
Hatua hiyo iliifanya serikali kuu kupinga uamuzi huo katika mahakama ya rufaa.
Bunge kwa sasa lipo mbioni kutunga sheria itakayosimamia utekelezaji wa mpango huo.