Home Habari Kuu Tutakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu, asema mbunge Geoffrey Ruku

Tutakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu, asema mbunge Geoffrey Ruku

Majaji wa mahakama kuu hiyo jana waliharamisha uteuzi wa mawaziri wasaidizi 50, katika uamuzi uliosema kuwa sheria na taratibu zilizoko hazikufuatwa katika uteuzi huo.

0
Mbunge wa Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku: Photo - Shirlyn

Mbunge wa Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku amesema mrengo wa Kenya Kwanza utakata rufaa uamuzi wa mahakama kuu ulioharamisha uteuzi wa mawaziri wasaidizi 50.

Akiongea hii leo na shirika la utangazaji nchini KBC Radio Taifa, Ruku alisema japo wanaheshimu uamuzi huo, Rais William Ruto anahitaji wasaidizi ili kufanikisha ahadi na ajenda yake kwa Wakenya.

“Tutakata rufaa juu ya hili swala la mawaziri wasaidizi (50 CAS) kwa sababu tunataka watu ambao wana mawazo na maono ya Rais Ruto katika kutekeleza yale ambayo aliahidi Wakenya, na wale wanaofahamu vizuri aliyowaahidi Wakenya ni wale aliokuwa akizunguka nao katika mikutano tofauti tofauti,” mbunge huyo aliambia Radio Taifa.

Majaji wa Mahakama Kuu hiyo jana waliharamisha uteuzi wa mawaziri wasaidizi 50, katika uamuzi uliosema kuwa sheria na taratibu zilizoko hazikufuatwa katika uteuzi huo. Majaji  walisema maoni ya wananchi kuhusu afisi hiyo hayakuchukuliwa ipasavyo kisheria.

Hata hivyo, mbunge huyo alitetea vikali uteuzi huo akisema nia ya awali ya rais ilikuwa ni kupunguza mzigo mkubwa unaowaelemea mawaziri katika wizara zao.

“Rais na mawaziri wanaamka mapema kufanya kazi hadi usiku wa manane, na wanahitaji kupumzika na watapumzika tu iwapo watapata wasaidizi,” alisema mbunge Ruku.

SOMA ZAIDI: Macky Sall amiminiwa sifa kwa kuridhia kustaafu

Aliwasihi vijana wawe na subira kwani rais ameweka mikakati kabambe ya kubuni nafasi zaidi kwa ajili yao.

“Vijana wasio na kazi wanashughulikiwa kikamilifu kupitia ile mipango iliyowekwa na serikali. Rais Ruto hakumaanisha kuwa atawapatia wanabodaboda kazi za waziri ama katibu,” Ruku aliambia Radio Taifa katika kipindi cha Zinga. 

 

 

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here