Home Habari Kuu Tutakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama, Seneta Cherargei asema

Tutakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama, Seneta Cherargei asema

0

Seneta wa kaunti ya Nandi Samson Cherargei amesema serikali itakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu uliotolewa leo Jumatatu mchana. 

Katika uamuzi huo, mahakama kuu ilitaja uteuzi wa makatibu waandamizi 50 kuwa uliofanywa kinyume cha katiba.

“Mahakama imekosea kwa kutoa uamuzi unaosema kuwa kubuniwa kwa nyadhifa za makatibu waandamizi kulikiuka katiba bila kuzingatia ustahili wa kesi hiyo,” alisema Seneta Cherargei.

“Tutakata rufaa dhidi ya uamuzi huo unaoenda kinyume cha maslahi ya umma na kanuni za haki.”

Wanasiasa Dr. Evans Kidero, Millicent Omanga, Isaac Mwaura, Nicholas Gumbo, Benjamin Washiali na Askofu Margaret Wanjiru ni miongoni mwa watu 50 waliokuwa wameteuliwa kwenye wadhifa huom ambao mahakama kuu imesema ulikiuka katiba.

Kwenye uamuzi wa jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo uliotolewa leo Jumatatu, mahakama ilibaini kwamba tume ya utumishi wa umma (PSC) ilikuwa imetenga nafasi 23 kwa ajili ya makatibu waandamizi lakini Rais aliteua 50.

Mnamo mwezi Machi, 2023, mahakama kuu ilizuia makatibu waandamizi 50 ambao walikuwa wameapishwa na Rais kuanza kazi hadi kesi iliyokuwa imewasilishwa na chama cha mawakili nchini, LSK na Katiba Institute isikilizwe na kuamuliwa.

Mahakama hiyo ilizuia pia makatibu hao kupokea mishahara na marupurupu.

Mahakama sasa inatoa ushauri kwa tume ya utumishi wa umma itekeleze uteuzi huo kwa njia inayowiana na katiba ya nchi.

Wakati wa kuunda afisi ya katibu mwandamizi chini ya serikali ya aliyekuwa wakati huo Rais Uhuru Kenyatta, pendekezo lilikuwa kwamba kuwe na katibu mwandamizi mmoja katika kila wizara.

Afisi hiyo iliondolewa na mahakama na kufufuliwa tena kutokana na pendekezo la Rais wa sasa William Ruto.

Ruto aliomba tume ya utumishi wa umma iongeze nafasi za makatibu waandamizi kutoka mmoja katika kila wizara hadi mmoja katika kila idara ya serikali.

Kuhusu suala la kuhususisha umma katika uteuzi wa makatibu waandamizi, ambalo ni hitaji la kikatiba, mahakama iliamua kwamba hata ingawa umma ulihusishwa, maoni ya umma hayakugusia nafasi 27 zaidi ambazo ziliongezwa.

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here