Home Kimataifa Baraza Jipya la Mawaziri: Tume ya Usawa wa Kijinsia yatathmini uwakilishi

Baraza Jipya la Mawaziri: Tume ya Usawa wa Kijinsia yatathmini uwakilishi

0
DKT. Joyce Mutinda, mwenyekiti NGEC
kra

Tume ya Usawa wa Kijinsia nchini, NGEC imesema kwamba Baraza la Mawaziri ambalo Rais William Ruto ameteua na ambalo linasubiri usaili wa bunge halijatimiza mahitaji ya sheria.

Katika taarifa iliyotiwa saini na mwenyekiti wa NGEC Joyce Mutinda, tume hiyo imechambua baraza hilo akiwemo Rais na Naibu wake kwa misingi ya jinsia, umri, maeneo yaliyotengwa na walemavu.

kra

Wateule wa kike ni 6 sawa na asilimia 28.57 huku wanaume katika baraza la mawaziri wakiwa 17 sawa na asilimia 71.43. Tume hiyo imesema kwamba, “Hatua hiyo sio sawa kwa mujibu wa kifungu nambari 27 sehemu ya 8 cha katika ya Kenya ya mwaka 2010.”

Sehemu hiyo inaelekeza kwamba katika kila kundi linaloteuliwa, wanachama wa jinsia moja hawafai kuzidi thuluthi mbili na kiwango hicho kingestahili kuwa wanaume 16 na wanawake saba.

Ili kutimiza hitaji hilo la katiba, NGEC inashauri serikali kuteua wanawake kujaza nafasi mbili zilizosalia moja ya waziri na nyingine ya mwanasheria mkuu.

Walemavu hawajawakilishwa kwa vyovyote kwenye baraza hilo la mawaziri huku vijana wakipata mwakilishi mmoja ambaye ni waziri mteule wa maji Eric Muriithi ambaye ana umri wa miaka 32.

Jamii zilizotengwa, zimepata uwakilishi wa asilimia 23.81 katika baraza hilo la mawaziri suala ambalo NGEC imepongeza.

NGEC sasa inashauri mamlaka ya uteuzi kuhakikisha kwamba kufikia mwisho wa uteuzi wa baraza la mawaziri iwe imetimiza mahitaji ya vifungu nambari 27, 54 na 55 vya katiba ya Kenya.

Website | + posts