Serikali ya kaunti ya Trans Nzoia imeshirikiana na kampuni moja ya Slovakia, katika juhudi za kuimarisha kilimo katika kaunti hiyo.
Akizungumza alipokutana na wawekezaji wa kampuni hiyo kupitia mtandao, Gavana wa kaunti hiyo George Natembeya, alitaja changamoto kuu inayowakumba wakulima wa eneo hilo kuwa bei ghali ya pembejeo za kilimo.
Hata hivyo, Gavana huyo alielezea matumaini kwamba changamoto za kilimo katika eneo hilo zitasuluhishwa ikiwa mpango kati ya serikali yake na kampuni ya ROKOSAN Organic Fertilizer kutoka Slovakia utafaulu.
Kulingana na Natembeya, uzalishaji mahindi umepungua katika eneo hilo, hali aliyotaja imesababishwa na udongo usio na rotuba ya kutosha na viwango vya chini vya mbolea.
“Uzalishaji wa mahindi umepungua katika kaunti ya Trans Nzoia, ambayo hutegemewa sana kwa chakula hapa nchini. Uzalishaji huo umepungua kutokaa magunia 40 hadi magunia kati ya 15-20 kwa kila ekari,” alisema Natembeya.
Wakikaribisha ushirikiano huo, wawakilishi wa kampuni hiyo ya ROKOSAN Marcelo Larramendy na Sonia Soloneski, walielezea nia ya ushirikiano zaidi katika kaunti hiyo.
Walidokeza kuwa shehena iliyo na magunia 20 ya mbolea za kiasili tayari zimefika humu nchini ili kufanyiwa majaribio na serikali ya kaunti hiyo pamoja na wakulima.