Serikali ya kaunti ya Trans-Nzoia, imechukua rasmi usimamizi wa makavazi ya Kitale, baada ya kutia saini mkataba wa maelewano na usimamizi wa taifa wa makavazi NMK, kwa lengo la kuboresha utoaji huduma.
Gavana wa kaunti ya Trans Nzoia George Natembeya, alisema uhamisho huo wa usimamizi wa makavazi kutoka kwa serikali kuu hadi serikali ya kaunti hiyo, ni hatua kubwa, miaka kumi baada ya kutekelezwa kwa ugatuzi.
Alipongeza hatua hiyo ya idara ya utamaduni na turathi ya kuhakikisha majukumu yaliyogatuliwa, yanahamishwa kwa serikali za kaunti, huku akitoa hakikisho kwamba kaunti hiyo itatekeleza jukumu hilo kwa uadilifu.
Katibu wa utamaduni na turathi Ummi Bashir, alisema kuhamishwa kwa makavazi ya kitaifa hadi kwa serikali za kaunti, hakutahujumu shughuli zilizopo, akithibitisha kuwa serikali za kaunti zitasimamia makavazi hayo kwa kuzingatia sheria.
Makavazi ya Kitale yako mjini Kitale na yana vifaa kutoka kwa jamii za humu nchini kama vile jamii ya wa Luhya, Maasai na Turkana, pia aina mbali mbali mbali ya mimea inapatikana katika makavazi hayo. Wanyama kama vile mamba, chui, kobe na nyoka wanapatikana hapo.
Kaunti zingine ambazo zimeorodheshwa kukabidhiwa makavazi ni pamoja na Wajir, Narok, Isiolo na Marsabit.