Home Habari Kuu Tovuti ya KUCCPS yafunguliwa kwa maombi ya kujiunga na vyuo vikuu na...

Tovuti ya KUCCPS yafunguliwa kwa maombi ya kujiunga na vyuo vikuu na vyuo

0
Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu.

Huduma ya kutoa nafasi kwa wanafunzi katika vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu nchini, KUCCPS imefungua tovuti yake kwa ajili ya maombi ya mwaka huu wa 2024.

Hatua hii inafuatia maelekezo ya Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu ambaye aliagiza KUCCPS ifungue tovuti hiyo ili kutoa fursa kwa waliofanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne mwaka 2023 kutuma maombi ya kujiunga na vyuo vikuu.

Taasisi nyingine ambazo nafasi zao zinapatikana kwenye tovuti ya KUCCPS ni pamoja na zile za kozi za kiufundi, taasisi za kutoa mafunzo kwa walimu na taasisi ya mafunzo ya utabibu, KMTC.

Tovuti hiyo imefunguliwa leo Februari 8, 2024 na itafungwa Februari 22, 2024.

Kulingana na Waziri Machogu, taasisi mbalimbali ziko tayari kuanza usajili wa wanafunzi wapya wa awamu ya mwaka 2024/2025.

Zinajumuisha vyuo vikuu 69, taasisi tatu za kutoa mafunzo kwa walimu wa sekondari, taasisi za mafunzo ya kiufundi 226 na taasisi 86 za KMTC.

Wanafunzi 201,073 waliofanya mtihani wa KCSE mwaka 2023 walipata alama ya C+ na zaidi na hivyo wamehitimu kujiunga na vyuo vikuu huku wengine 694,231 wakihitimu kwa kozi za kiufundi, kozi za ualimu na za utabibu.

KUCCPS itaandaa kampeni za uhamasisho kuhusu usajili wa mwaka 2023 katika vituo 262 kote nchini ambavyo ni taasisi 210 na vituo vya huduma 52, kwa lengo la kusaidia wanafunzi kuchagua kozi wanazotaka kusomea.

Wanafunzi watakaojiunga na vyuo vikuu na taasisi nyinginezo mwaka 2023 watakuwa kundi la pili kufaidika kutokana na mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu.

KUCCPS inahimizwa kuharakisha mchakato wa usajili ili kuhakikisha wanafunzi wanajiunga na taasisi zao mapema.

Website | + posts