Home Habari Kuu Timu za kitaifa za Talanta hela zatangazwa

Timu za kitaifa za Talanta hela zatangazwa

0
Waziri wa Michezo Ababu Namwamba

Waziri wa michezo Ababu Namwamba ametoa orodha ya wachezaji walioteuliwa kujiunga na timu za kitaifa za Talanta Hela.

Timu hizo ni za wasichana na wavulana, za wachezaji walio chini ya umri wa miaka 17 na wachezaji walio chini ya umri wa miaka 20.

Kulingana na waziri Namwamba timu hizo sasa ziko tayari kupeperusha bendera ya taifa la Kenya Ughaibuni huku wachezaji wakijipatia riziki.

Waziri alielezea kwamba walianzisha mfumo endelevu wa kutambua na kukuza talanta za michezo kutoka shuleni kupitia kinyang’anyiro cha Talanta Hela kinachohusisha kaunti mbali mbali.

Huku akikiri kwamba sehemu zote za Kenya zimewakilishwa kwenye timu hizo, Namwamba alisema zinaandaliwa kuanza mazoezi ya kiwango cha juu.

Zinaandaliwa pia kwa mashindano ya soka kwa wachezaji wa umri mdogo almaarufu MICFootball – International mwisho wa mwaka ujao nchini Uhispania.

Namwamba alisema wataendelea ktoa nafasi kwa walio na talanta ambao wanaishi nchini na ughaibuni, akiongeza kusema kwamba Kenya itashiriki mashindano ya kombe la dunia kwa wachezaji wa umri wa chini ya miaka 17 na miaka 20.

“Tumejitolea kuunda timu bora ya taifa hili Harambee Stars kwa ajili ya kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2027 na kombe la dunia mwaka 2030.” alisema waziri Namwamba kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.

Alishukuru taasisi ya michezo nchini Kenya Academy of Sports kwa kuongoza mashindano ya Talanta Hela pamoja na wahusika wote wakiwemo makocha.