Home Kimataifa Thailand huenda ikawa nchi ya tatu barani Asia kukubalia ndoa za jinsia...

Thailand huenda ikawa nchi ya tatu barani Asia kukubalia ndoa za jinsia moja

0

Taifa la Thailand huenda likawa taifa la tatu katika bara Asia kukubalia ndoa kati ya watu wa jinsia moja, hii ni baada ya bunge la chini nchini humo kupitisha mswada wa sheria ya kukubalia ndoa hizo.

Katika kikao cha leo Jumatano, wabunge wa bunge hilo walipigia kura mswada huo ambapo 400 waliuunga mkono huku 10 pekee wakikosa kukubaliana nao.

Mswada huo sasa unasubiri kupitishwa na bunge la seneti kabla ya kutiwa saini kuwa sheria na mfalme wa nchi hiyo. Iwapo mfalme ataitia saini kuwa sheria itaanza kutumika siku 120 baadaye.

Kabla ya shughuli ya kupigia kura mswada huo, mwenyekiti wa kamati ya bunge hilo kuhusu sheria Danuphorn Punnakanta,alitoa mwaliko kwa wabunge wenza kuandikisha historia akisema kama kamati walichukua hatua hiyo kwa ajili ya watu wote wa Thai na kuhakikisha usawa katika jamii.

Mswada huo unapendekeza mabadiliko katika namna wanandoa wanavyorejelewa bila kuzingatia jinsia ili kujumuisha wapenzi wa jinsia moja.

Nchi ya Thailand huwa inakaribisha wapenzi wa jinsia moja lakini wanaharakati wamekuwa wakijitahidi sana kupambana na unyanyapaa katika jamii.

Mahakama ya katiba nchini humo iliamua mwaka 2020 kwamba sheria ya ndoa ambayo inatumika kwa sasa inayotambua ndoa kati ya mwanaume na mwanamke pekee ni halali kikatiba. Hata hivyo mahakama hiyo ilipendekeza kupanuliwa kwa sheria hiyo ili kujumuisha haki za makundi yaliyotengwa.

Kwa sasa mataifa ya Taiwan na Nepal ndiyo pekee yanayotambua na kukubalia ndoa za jinsia moja.

Website | + posts