Wenyeji Ivory Coast walianza vyema makala ya 34 ya kipute cha kombe la mataifa ya Afrika, AFCON kwa ushindi wa mabao mawili kwa bila dhidi Guinea Bissau.
Pambano hilo la kundi A lilisakatwa ugani Alassane Ouatara mjini Abidjan Jumamosi usiku.
Seko Fofana alipachika bao la kwanza kunako dakika ya nne akiunganisha pasi ya Frankie Kessie na kuwanyanyua mashabiki wa nyumbani.
Jean-Philippe Krasso alihitimisha kibarua kwa tembo hao akifunga bao la pili baada ya kumpokonya mpira beki wa Guinea Bissau.
Awali, kulikuwa na sherehe kabambe ya kufungua mashindano ikiongozwa na Rais wa FIFA Gianni Infantino na kinara wa CAF Dkt. Patrice Motsepe.
Motsepe alielezea matumaini yake ya Ivory Coast kuandaa mashindano ya kufana.
Kundi la Magic System na msanii kutoka Nigeria Yemi Alade waliporomosha burudani.
Kindumbwendumbwe hicho ktaingia siku ya pili Jumapili jioni Nigeria wakikabiliana na Equatorial Guinea kuanzia saa kumi na moja kundini A.
Saa mbili usiku itakuwa zamu ya mechi za kundi B, Misri wakikumbana na Musumbiji saa mbili usiku huku Ghana wakihitimisha mzunguko wa kwanza dhidi ya Black Stars ya Ghana kuanzia saa tano usiku.
Mechi zote zitapeperushwa na runinga ya KBC Channel 1 na kutangazwa kupitia idhaa zote 14 za KBC.