Home Kaunti Tatizo la vifo vya kina mama na watoto Trans Nzoia

Tatizo la vifo vya kina mama na watoto Trans Nzoia

0

Kaunti ya Trans Nzoia inakumbwa na idadi ya juu ya vifo vya kina mama na watoto. Hata baada ya serikali na wahudumu wa afya kuhimiza jamii kwenda hospitalini kwa matibabu, kaunti hiyo bado inashuhudia vifo ambavyo vingezuilika.

Anne Kipsuto, mshirikishi wa mipango katika shirika la USAID AMPATH Uzima, anasema kaunti hiyo imepoteza kina mama na watoto zaidi ya 20 kutokana na matatizo ya kujifungua tangu Januari.

Watoto wengine wapatao 800 wameaga dunia kabla ya kukamilisha siku 28 za maisha yao.

Kipsuto alikuwa akizungumza wakati wa mkutano wa uhamasisho kuhusu afya katika hoteli moja mjini Kitale, kaunti Trans Nzoia uliojadili viwango na ubora na uboreshaji.

Mkutano huo uliofadhiliwa na USAID AMPTH Uzima, uliangazia haja ya kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Kipsuto alisisitiza umuhimu wa kuafikia malengo ya kiafya yanayotakiwa kwa watu binafsi na kwa umma.

Takwimu za kaunti ya Trans Nzoia na za Kenya kwa jumla zinaonyesha visababishi vya vifo vya kina mama ambavyo vinaweza kuzuiwa kama vile kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua, kuvuja damu kabla ya kujifungua, shindikizo la damu wakati wa ujauzito na mishtuko, uchungu wa kujifungua uliokwazwa na kukatika kwa mfuko wa uzazi.

Kuhusu vifo vya watoto wanaozaliwa, visababishi vikuu vya vifo ni kukithiri kwa magonjwa, kutokua kikamilifu, kunyongwa, kuhara, kukosa lishe bora na nimonia.

Kenya imejitolea kimataifa kupunguza vifo vya kina mama na watoto kwa mfano kupitia kukubali mpango wa kumaliza vifo hivyo.

Kipsuto aliomba kaunti hiyo ijibidiishe katika kuafikia malengo ya kimataifa ya upatikanaji wa huduma za kina mama wajawazito kwa kiwango cha asilimia 90, upatikanaji wa wataalamu wa kusaidia kina mama kujifungua kwa kiwango cha asilimia 90 na upatikanaji wa huduma za kina mama na watoto baada ya kujifungua kwa kiwango cha asilimia 80.

Alisisitiza pia umuhimu wa kuhakikisha hospitali za Level 2 na 3 zinapata mashine za kusaidia watoto kupumua kwa kiwango cha asilimia 65 na asilimia 85 ya hospitali ziwe zimetimiza masharti ya kutunza kina mama wanaojifungua na watoto wanaozaliwa.

Buluma, ambaye ni mshirikishi wa mipango ya utoaji chanjo, aliangazia umuhimu wa huduma bora akisisitiza kuhusu viwango vinane vya ubora vya shirika la afya ulimwenguni.

Mkutano huo uliishia wito kwa wadau wote kushirikiana kuboresha huduma za afya kwa kina mama na watoto katika kaunti ya Trans Nzoia.

Website | + posts