Home Habari Kuu Kenya kuendelea kushuhudia mvua kubwa

Kenya kuendelea kushuhudia mvua kubwa

0
Maeneo mengi ya nchi yanaendelea kushuhudia mvua kubwa.

Sehemu nyingi za taifa hili zitaendelea kushuhudia mvua kubwa, kulingana na idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini.

Utabiri uliotolewa siku ya Ijumaa na idara hiyo wa siku saba zijazo, kutakuwa na dhoruba katika sehemu za nyanda za juu za Mashariki na Magharibi  mwa Rift Valley, eneo la Pwani na Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Aidha kulingana na utabiri huo maeneo kadhaa ya nchi yatashuhudia mvua nyakati za asubuhi na alasiri, huku ngurumo za radi zikishuhudiwa katika kaunti kadhaa kote nchini.

Kaunti hizo ni pamoja na Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia na Pokot Magharibi.

Viwango vya juu vya joto katika kipindi hicho vitafika nyuzi 29 huku viwango vya chini vya joto vikiwa nyuzi 12.

Kaunti ya Nairobi na nyanda za juu Mashariki mwa Rift Valley, zitashuhudia mvua nyakati za asubuhi katika maeneo kadhaa.

Kaunti za Kaskazini Mashariki mwa nchi za Marsabit, Mandera, Wajir, Garissana Isiolo, zitashuhudia mvua nyakati za asubuhi, huku rasharasha zikishuhudiwa alasiri. Viwango vya juu vya joto katika kaunti hizo vitafika nyuzi 32 na vya chini vikiwa nyuzi 12.

Kaunti za Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado na Taita Taveta, pia zitashuhudia mvua nyakati za ashubuhi na alasiri.

Kulingana na utabiri huo, kaunti za Mombasa, Tana-River, Kilifi, Lamu na Kwale zitashuhudia mvua majira ya asubuhi, huku rasharasha za mvua zikishuhudiwa katika kaeneo kadhaa alasiri.

Website | + posts