Mabingwa mara tatu wa kombe la mataifa ya Afrika, AFCON Super Eagles kutoka Nigeria, wametinga nusu fainali ya kipute cha mwaka huu baada ya kuilaza Angola bao moja kwa bila Ijumaa jioni.
Mkwangurano huo ulisakatwa katika uga wa Stade Félix Houphouët-Boigny mjini Abidjan.
Super Eagles walihitaji goli la Ademola Lookman kunako dakika ya 41 kipindi cha kwanza, akiunganisha pasi rojorojo kutokea pembeni ksuhoto ikichongwa na Moses Simon.
Licha ya Palancas Negras ukipenda swara wa Angola kujizatiti kurejea mchezoni, hali ilikuwa tete kwao na kulazimika kumeza shubiri wakisubiri kukwea pipa Jumamosi kurejea kwao Luanda.
Nigeria wanaowinda kombe la AFCON kwa mara ya nne watasubiri mshindi wa robo fainali ya Jumamosi usiku baina ya Afrika Kusini na Cape Verde, ili kupimana ubabe katika nusu fainali Jumatano ijayo.