Home Kimataifa Taa za kurembesha gari marufuku Iringa Tanzania

Taa za kurembesha gari marufuku Iringa Tanzania

0

Taa ambazo wamiliki wa magari hujiongezea kwenye magari yao kama njia ya kuzirembesha zimepigwa marufuku katika mkoa wa Iringa nchini Tanzania.

Msimamizi wa masuala ya usalama barabarani katika mkoa huo Mosi Ndozero ametangaza hayo akisema magari yanafaa kusalia na mwonekano halisi.

Ndozero alitoa matamshi hayo wakati alikuwa akitekeleza doria ya usalama barabarani ambapo aliwataka waliojiongezea taa kwa magari waziondoe mara moja.

Kulingana naye taa hizo husumbua macho ya madereva wengine barabarani ambapo wanapata upofu wa muda mfupi suala ambalo huenda likasababisha wapoteze mwelekeo na kusababisha ajali.

Mwanga unaobadilika badilika wa taa hizo alisema ni hatari kwa macho huku akifananisha magari yenye taa kama hizo na nyumba zinazotembea au kumbi za disco.

Mkuu huyo wa usalama barabarani Iringa aliwataka madereva pia kukoma kuhamisha nambari za usajili wa gari kutoka katikati ya gari zilikowekwa mwanzo na kuziweka pembeni.

Onyo hilo alilielekeza hasa kwa madereva wa malori akisema inakuwa vigumu kutambua gari nambari hizo zinapohamishwa.