Home Burudani Steve Harvey akanusha madai ya kutengana na mkewe

Steve Harvey akanusha madai ya kutengana na mkewe

0

Mchekeshaji na mtangazaji Steve Harvey wa Marekani amekanusha madai kwamba yeye na mke wake Marjorie wametengana na kwamba watatalikiana.

Akizungumza kwenye tamasha ya InvestFest awamu ya mwaka 2023, Harvey alisema, “Sijui ni nini mnafanya na mnasema lakini tafuteni la kufanya kwa sababu sisi tuko sawa” na akaongeza kwamba hana muda wa kuzungumzia mambo ya uongo.

Taarifa kuhusu matatizo katika ndoa ya Steve Harvey zimesheheni mitandao ya kijamii kwa muda sasa ingawa hakuna chanzo kikuu cha taarifa kilichothibitisha na hivyo zikatiliwa shaka na sasa imebainika kwamba haikuwa kweli.

Habari hizo za uongo zilizoanzishwa na watu mitandaoni zilidai kwamba Marjorie alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mlinzi wa mume wake.

Ilidaiwa pia kwamba Marjorie ambaye amekuwa kwenye ndoa na Harvey tangu mwaka 2007 amedai nusu ya mali ya Harvey kwenye talaka.

Marjorie naye alitumia akaunti yake ya mtandao wa Instagram kukanusha taarifa za utengano ambapo alichapisha kifungu cha Biblia 1 Petero 23 : “Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki”.

Aliongeza kusema kwamba yeye na mume wake hawana tabia ya kujibu mambo ya uongo lakini imebidi kwa sababu ya kuwa watu maarufu na anaelewa kwamba aliyejaliwa mengi, mengi hutarajiwa kutoka kwake. Alisambaza picha ya tovuti moja ambayo inatoa mafunzo ya jinsi ya kusimamia mambo ya uongo huku akihimiza wafuasi wake kusoma.

Website | + posts