Home Habari Kuu Spika Wetangula akutana na waziri wa mambo ya nje wa Yemen

Spika Wetangula akutana na waziri wa mambo ya nje wa Yemen

0
Spika Wetangula na waziri Ahmed Bin Mubarak

Hivi leo spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula amefanya mkutano na waziri wa mambo ya nje wa Yemen Ahmed Bin Mubarak, aliyemzuru katika afisi yake kwenye majengo ya bunge.

Mkutano huo ambao unaashiria uhusiano mwema na wa muda mrefu ambao umekuwepo kati ya Yemen na Kenya unalenga kuimarisha uhusiano huo hata zaidi hasa katika biashara ya chai na kahawa.

Kenya inatambua Mashariki ya Kati kama soko muhimu kwa mazao yake na ushirikiano huo unalenga kuboresha biashara na kuchochea uwekezaji na kubuniwa kwa nafasi za ajira nchini Kenya.

Kulingana na Wetangula Kenya ni kiingilio muhimu cha eneo zima la Afrika Mashariki ndiposa ina sera ya kimakusudi ya kuhusiana na marafiki wa Mashariki ya Kati kwa kutambua umuhimu wao kama soko la mazao ya Kenya ya kahawa na Chai na pia ni kituo muhimu cha usafirishaji wa bidhaa hadi masoko mengine.

“Sisi kama Kenya tuko na sera ya kimakusudi ya kuhusiana na marafiki wetu katika eneo la Mashariki ya kati, ambayo ni muhimu kwa biashara na ni soko kubwa kwa mazao yetu ya chai na kahawa.” alisema spika Wetangula akiongeza kwamba hata wakati ambapo watu wa eneo hilo hawatumii bidhaa za Kenya, ni muhimu katika kufikia masoko mengine.

Wetangula alihimiza watu wa Yemen wawekeze nchini Kenya, washiriki uzalishaji chakula na kuanzisha vituo vya kibiashara nchini jambo ambalo hatimaye litasababisha kupatikana kwa fursa za biashara na za ajira kwa wakenya.

Spika alidhihirisha matumaini ya amani kupatikana nchini Yemen kwa sababu uthabiti wake unaathiri Kenya moja kwa moja.

“Amani katika Yemen ni amani nchini Kenya na kama hakuna amani Yemen basi Kenya itaathirika kwa njia nyingi.” alisema Wetangula.

Waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na naibu spika wa bunge la kitaifa Glady Boss, balozi wa Yemen Abdulsalam Alawi na afisa wa ubalozi wa Yemen Sheikh Saleh Shigog.

Website | + posts