Home Kimataifa Spika Wetang’ula ahudhuria kongamano la 27 la maspika wa jumuiya ya madola

Spika Wetang’ula ahudhuria kongamano la 27 la maspika wa jumuiya ya madola

0

Spika wa bunge la taifa Moses Masika Wetang’ula yuko jijini Kampala nchini Uganda ambako aliwasili jana jioni kwa ajili ya kongamano la 27 la maspika na maafisa wakuu wa mabunge ya nchi za jumuiya ya madola.

Anatarajiwa kuhutubia kongamano hilo kuhusu jukumu la mabunge katika kushugulikia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kulinda mazingira.

Alipowasili jana, Wetang’ula alilakiwa na naibu spika wa bunge la Uganda Thomas Tayebwa, mbunge Opolot Fred na balozi wa Kenya nchini Uganda Meja Jenerali George Owino.

Kongamano la mwaka huu la maspika na maafisa wakuu wa mabunge katika jumuiya ya madola linaandaliwa kati ya tarehe 3 na 6 Januari, 2024 waandalizi wakiwa bunge la Uganda.

Mada nyingine zinazotarajiwa kuzungumziwa kwenye kongamano hilo ni pamoja na mabunge jumuishi, mipango ya ulinzi kwa wabunge na mabunge pamoja na fursa zilizopo kati ya wabunge wa jumuiya ya madola.

Lengo kuu la kongamano hilo ni kuhimiza uadilifu kwa upande wa maspika na maafisa wengine wakuu wa mabunge. Ni jukwaa bora pia la upatikanaji wa ujuzi na uelewa wa uhuru wa kuchagua bungeni ili kuendeleza taasisi mbali mbali za bunge.

Kongamano hilo lilianzishwa mwaka 1969 na huwa linaandaliwa kila baada ya miaka miwili na hukutanisha maspika na maafisa wakuu wasimamizi wa mabunge ya kitaifa ya nchi huru za Jumuiya ya Madola.

Spika Wetangula ameandamana na Naibu karani wa bunge la taifa Serah Kioko na naibu karani wa bunge la seneti Mohammed Ali.

Website | + posts