Home Habari Kuu Spika Wetang’ula ahudhuria hafla ya Moran kuhitimu kuwa wazee

Spika Wetang’ula ahudhuria hafla ya Moran kuhitimu kuwa wazee

0

Spika wa bunge la Taifa Moses wetang’ula alikuwa mgeni rasmi wa hafla ya vijana wapatao 3,000 wa jamii ya Maasai almaarufu Moran ya kuhitimu kuwa wazee, katika kijiji cha Rutian, eneo bunge la Narok Kaskazini, kaunti ya Narok.

Wetang’ula ambaye alikuwa ameandamana na wabunge kadhaa, alisema hafla hiyo ni muhimu katika malezi na makuzi ya vijana wa jamii ya Maasai.

Alisifia jamii hiyo kwa kujitolea kuendeleza utamaduni huku akiwakumbusha kwamba utamaduni wa Maasai kwa muda mrefu umechukuliwa kuwa utambulisho wa taifa la Kenya.

“Ulimwengu huwa unaambatanisha Kenya na jamii ya Maasai hasa utamaduni wao,” alisema Wetang’ula huku akiahidi kwamba bunge limejitolea kuendeleza utamaduni wa nchi, utamaduni wa jamii ya Maasai ukiangaziwa zaidi.

Spika huyo alitumia hafla hiyo kuomba serikali itekeleze ufurushaji wa watu kutoka kwa msitu wa Mau kwa njia ya utu kwa kuzingatia haki za binadamu.

Alisema anaunga mkono kikamilifu juhudi za serikali za kuhifadhi msitu wa Mau lakini ufurushaji haufai kusababisha uharibifu wa aina yoyote.

Kiongozi huyo aliwakumbusha watu wa jamii ya Maasai kwamba eneo la vyanzo vya maji ni muhimu sana kwao kuliko jamii nyingine na hivyo ni lazima wajitolee kulinda msitu huo.

Wabunge waliokuwa kwenye hafla hiyo ni pamoja na Elijah Memusi Kanchory wa Kajiado ya kati, Zaheer Jhanda wa Nyaribari Chache na Japheth Nyakundi wa Kitutu Chache Kaskazini.

Website | + posts